Pata taarifa kuu
BRAZIL 2014

Serikali ya Ghana yakodi ndege kuwapelekea marupurupu wachezaji wa "The Black Stars"

Serikali ya Ghana imetuma ndege ya kukodi ikiwa imebeba fedha taslimu zaidi ya Dola Milioni 3 kwenda Brazil kuwalipa wachezaji wa timu ya taifa ya The Black Stars inayoshiriki katika michuano ya soka ya kombe la dunia.

Kevin Prince Boateng wa Ghana akimenyana na kakake  Jerome Boateng, wa Ujerumani
Kevin Prince Boateng wa Ghana akimenyana na kakake Jerome Boateng, wa Ujerumani REUTERS/Mike Blake
Matangazo ya kibiashara

Naibu Waziri wa Michezo nchini humo Joseph Yamin amekiambia kituo cha redio cha Citi FM jijini Accra kuwa ndege hiyo iliondoka Accra siku ya Jumanne ikiwa na fedha hizo kwenda Brazil.

Aidha, Naibu Waziri huyo ameongeza hatua hiyo ilichukuliwa baada ya wachezaji wa Black Stars kukataa kutumiwa fedha zao kutokea jijini Accra kwa mfumo mwingine na badala yake walitaka kulipwa wakiwa Brazil.

“Tumelazimika kutumia njia hii kuwatumia fedha zao hali ambayo imewafanya kutopata marupurupu yao siku ya leo.,” Waziri huyo alinukuliwa akisema.

“Serikali inatambua umuhimu wa soka hapa nchini na ni jukumu letu, kuhakikisha kuwa wachezaji wetu wanapata malipo yao,” aliongezea

Kiungo wa kati wa Ghana Sulley Muntari akioneshwa kadi ya njano
Kiungo wa kati wa Ghana Sulley Muntari akioneshwa kadi ya njano REUTERS/Laszlo Balogh

Shirikisho la soka nchini Ghana limesema, rais wa nchi hiyo John Dramani Mahama awali aliwahakikishia wachezaji hao kuwa watapata fedha zao kwa wakati.

Serikali ya Ghana inasema imelazimika kutumai fedha zake kuwalipa wachezaji hao kila siku, na zitarudishwa na Shirikisho la soka nchini humo, baada ya shirikisho la soka duniani FIFA kutuma fedha za Ghana kushiriki katika michuano hiyo baada ya kumalizika kwa kombe la dunia.

The Black Stars bado wana nafasi ya kufika katika hatua ya 16 bora ikiwa wataishinda Ureno wakati wa mchuano wao wa kutamatisha kundi lao Alhamisi hii.

Ghana wana alama moja sawa na Ureno, huku timu zingine zilizo katika kundi hilo Marekani na Ujerumani zikiwa na alama 4.

Asamoah Gyan akifanya mazoezi kabla ya mchuano wa Alhamisi dhidi ya Ureno
Asamoah Gyan akifanya mazoezi kabla ya mchuano wa Alhamisi dhidi ya Ureno REUTERS/Toru Hanai

Juma hili, kulikuwa na madai kutoka gazeti la Uingereza la Daily Telegraph likimtuhumu rais wa Shirikisho la soka la Ghana Kwesi Nyantakyi kukubali kupanga matokeo ya michuano ya kirafiki baada ya kukamilika kwa michuano ya kombe la dunia, tuhma ambazo zimekanushwa na rais huyo.
 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.