Pata taarifa kuu
WRC Safari Rally 2024

Safari Rally yatazimiwa kuwa kwenye 'njia sahihi' kuinuka ngazi za juu duniani

Nairobi – Naibu rais wa mchezo wa magari barani Afrika, FIA, Rodrigo Ferreira Rocha amesifia maandalizi na mashindano ya magari ya Safari Rally kama mojawapo ya mikondo kumi na tatu katika msururu wa mashindano ya kuendesha magari duniani (WRC). Aidha ameelezea mbinu za kuongeza idadi ya madereva wa kiafrika kushiriki mikondo mingi na namna ya kuinua mchezo huo barani Afrika.

Wachez densi wa jamii ya Maasai kwenye mstari wa kumaliza mashindano katika hatua ya Hell's Gate
Wachez densi wa jamii ya Maasai kwenye mstari wa kumaliza mashindano katika hatua ya Hell's Gate © WRC
Matangazo ya kibiashara

Safari Rally ndio mkondo pekee wa WRC unaoandaliwa barani Afrika.

“Umeona jinsi inathaminiwa na wakenya, anga na msisimko wake ni jambo sijawahi kuona popote ulimwenguni,” alisema Rodrigo.

“Tunajivunia waandalizi wa Safari Rally, walishughulikia kila changamoto na kuweza kuiweka kwenye jukwaa la kimataifa kama hafla ya kiwango cha kimataifa. Wale ambao walikuwa na shaka kama Kenya inaweza kuwa mwenyeji mwaka huu, kutoka kwangu tunatupilia mbali shaka hizo. Sasa kuna nafasi ya kuboresha.”

Tayari madereva wa magari walipaza sauti zao kwa waandalizi kuongeza siku za mashindano kutoka nne hadi wiki nzima wakidai muda mchache wa kujiandaa. Kulingana na Rodrigo, ikiwa promota wa Safari Rally, vitengo husika vya FIA vya usalama na kiufundi vitakubaliana kuongezwa kwa siku za mashindano basi ina maana moja tu “tuko kwenye njia sahihi ya kuleta tukio hili katika hatua za juu zaidi.”

Dereva Gus Greensmith wa Skoda Fabia na msaidizi wake Jonas Andersson walioshinda kitengo cha WRC2
Dereva Gus Greensmith wa Skoda Fabia na msaidizi wake Jonas Andersson walioshinda kitengo cha WRC2 © WRC

Rodrigo pia anakiri huu ndio mkondo mgumu zaidi kwenye kalenda ya WRC  akisisitiza si bure unaitwa ‘Safari’ kwa sababu ya vigezo vya wanyama, maeneo wazi na asili pamoja na barabara zenye vumbi na matope ambazo hutoa changamoto kubwa kwa madereva.

“Hakika, unahitaji ujuzi halisi ili kutoboa mkondo huu,” aliainisha Rodrigo.

Ndio, huu ni mkondo pekee unaofanyika Afrika. Lakini je, baada ya mkondo huu ni madereva wangapi wa kiafrika hushiriki mikondo inayofuata?

Katika historia miaka miwili iliyopita, ni mkenya McRae Kimathi ambaye alijaribu kushiriki mikondo mingine kando na Safari Rally. Alishiriki Rally Sweden 2022, 2022 Ralle de Portugal na 2022 Croatia Rally.

McRae Kimathi (kulia) baada ya kuibuka wa tatu kwenye WRC3 mwaka 2022
McRae Kimathi (kulia) baada ya kuibuka wa tatu kwenye WRC3 mwaka 2022 © Wizara ya Michezo Kenya

Lipi la kufanywa ili madereva kutoka Afrika washiriki mikondo mingi ya WRC?

“Unajua ni gharama kubwa sana kushiriki misururu mingi,” alibainisha Rodrigo. “Kutoa gari Afrika hadi bara Uropa ni gharama kubwa, ukizunguzmai Afrika gharama inapanda zaidi sababu hatuna wataalamu wa idara tofauti tofauti wa kutuongoza kuelekea mashindanoni.”

“Timu zinafaa kuhusisha wadhamini ili kufanikiwa na nahisi tunakosa hayo tu sababu talanta zipo.”

FIA haiwezi kutoa udhamini kwa madereva ila inatoa nafasi wa kila dereva kushiriki kwenye huu mchezo ila: ushirikiano sahihi na taasisi sahihi za fedha itasaidia.

Safari Ndefu ila Mwisho mwema ndio Hoja

"Ni mapema mno kuzungumzia mafanikio sababu huwa napata kejeli nyingi sana kwa kazi yangu ila kwa mara ya kwanza tumeanzisha mashindano ya mchujo barani Afrika iliyofanyika mapema mwaka huu ambapo mataifa saba yalituma madereva wao nchini Afrika Kusini."

"Pia tumeanzisha mradi wa mashindano kufanyika mahali popote afrika na tumetoa vifaa hitajika kwa wanachama wetu wote kuanza kujiandaa na kujiweka sawa. Pia tumeanzisha mfumo wa kidijitali wa mashindano ya magari ambapo tunaweza kuunganisha wanachama wote."

Rodrigo anasema ana nia ya kufanya mashindano ya magari ya Afrika iwafikie madereva wote wenye talanta na kuifanya kuwa tamu zaidi kwa wadhamini, mashabiki na madereva. "Lakini pia kuanza kwa michezo mingine mipya kama vile Gymkhana, drifting, carstalone ambapo naamini Afrika inaweza kubobea katika michezo hiyo."

Adhari ya Mfumo mpya wa Alama

Kabla ya Safari Rally ya mwaka huu kuanza, FIA ilitoa mfumo mpya wa kuwapa alama madereva kuelekea hatua ya mwisho ya Hell’s Gate. Mara nyingi madereva walionekana kujilinda siku ya Ijumaa kwa kupunguza kasi ili kulinda magurudumu yao kabla ya siku mwisho ili kuzoa alama nyingi.

Washindi wa 2024 Safari Rally, Kalle Rovanpera (1), Takamoto Katsuta (2), Adrien Formaux (3)
Washindi wa 2024 Safari Rally, Kalle Rovanpera (1), Takamoto Katsuta (2), Adrien Formaux (3) © WRC

Dereva msaidizi Adnan Din, ambaye alimwongoza kijana Hamza Anwar kwenye mashindano ya chipukizi ya WRC alitabiri Safari Rally ya mwaka 2024 yenye ushindani zaidi.

"Nadhani ni ya ajabu. Sasa wafanyakazi wa WRC wanapaswa kufanya kazi kwa bidii zaidi na kupita siku zote mbili ili kupata alama muhimu. Pia ina manufaa zaidi kwa timu ambayo imepitia hatua zote. Binafsi, nadhani itafanya WRC Safari Rally ya mwaka huu kuwa kitu cha kutazamia.”

Bingwa wa zamani wa Kenya wa kuendesha magari ya Two Wheel Drive, Dennis Mwenda almaarufu "Dere Mwenda" alisema: "Lo! Hiki ni kigezo kikubwa cha kubadilisha mchezo ambacho kitachochea matukio ikijumuisha Safari Rally yetu kuwa ya kusisimua na yenye ushindani zaidi."

Mwenda aliendelea: “Kuongoza Jumamosi bila shaka kutakuwa jambo la manufaa zaidi kwa madereva wa kitengo cha kwanza. Hakutakuwa na kupunguza kasi ili kuokoa matairi kwa hatua ya nguvu. Itakuwa mafanikio ya vita kuongeza pointi."

Hili lilibainika wazi katika siku ya mwisho ya mashindano ambapo mshindi wa Safari Rally 2024 Kalle Rovanpera alijizolea alama 20 kwa jumla, ila nafasi ya pili Takamoto Katsuta alipata alama 18, alama moja chini ya Thierry Neuville ambaye alimaliza nafasi ya tani kwenye Safari Rally.

Naibu rais wa FIA Afrika, bwana Rocha alikuwa na kauli kuhusiana na mfumo huo mpya wa kutoa alama kwa madereva.

“Hii ni moja ya mambo tunayoyaona kama maendeleo ya kazi. Hakutakuwa na suluhisho bora kabisa, lazima tujaribu uwezekano wote kuleta usawa kwa kila mtu.”

“Kama tayari mambo yalikuwa sawa tusingekuwa tunafanya mabadiliko yoyote, bila shaka tunaamini itaimarisha ushindani,” alisisitiza Rodrigo.

Kwenye suala la kukuza mchezo huu barani Afrika, Rodrigo Rocha anasema kuna programu ya Cross Country ambayo ni njia mojawapo ya kutoa zana kwa mashirikisho ya Afrika, ili kuwafikia madereva na kuwapa mwanga zaidi mashindanoni. Pia kushiriki kwenye mchujo wa Afrika utakaofanyika mwaka ujao ni njia nyingine ya kukuza mchezo huu na kuifanya kurejea kwa kishindo. 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.