Mgogoro Ukraine: jeshi latumwa katika miji muhimu
Rais wa Ukraine Petro Poroshenko ameliamuru jeshi, kuimarisha usalama katika miji ya kusini na Mashariki mwa nchi hiyo kwa hofu ya kuzuka kwa uasi mpya.
Imechapishwa:
Rais Poroshenko ametaja miji inayostahili kupewa ulinzi mkali ni pamoja na Mariupol, Berdyansk, Kharkiv na Kaskazini mwa jimbo la Luhansk.
Kiongozi huyo wa Ukraine ametoa agizo hilo baada ya kukutana na viongozi wa usalama katika majimbo ya Donetsk na Luhansk yanayodhibitiwa na waasi.
Poroshenko pia amesisitiza kuwa serikali yake bado ina nia ya kutekeleza mpango wa amani ulioafikiwa mwezi Septemba mwaka huu mjini Minsk nchini Belarus ili kumaliza mzozo mashariki mwa nchi hiyo.
Katika hatua nyingine, amelaani uchaguzi uliotokea mashariki mwa nchi hiyo na kuungwa mkono na Urusi na kusisitiza kuwa ulikuwa kinyume na sheria.
Tayari viongozi wa majimbo ya Donetsk na Luhansk waliochaguliwa mwishoni mwa juma lililopita wameapishwa.