Pata taarifa kuu
Mashindano ya Shule za Afrika

Uganda kuwakilisha Afrika Mashariki Michuano ya CAF Shule za Afrika mwaka 2024

NAIROBI – Shule ya upili ya wasichana ya Kawempe Muslim na ya wavulana ya St Mary’s Kitende kutoka Uganda ndio watakaowakilisha ukanda wa Afrika Mashariki katika mashindano ya CAF shule za Upili itakayofanyika mwaka ujao mwezi Aprili. 

St Mary's Kitende ya wavulana ya Uganda baada ya kukabidhiwa taji la CECAFA shule za Upili jijini Nairobi 13.12.2023
St Mary's Kitende ya wavulana ya Uganda baada ya kukabidhiwa taji la CECAFA shule za Upili jijini Nairobi 13.12.2023 Football Kenya Federation
Matangazo ya kibiashara

Michuano hiyo ya kufuzu ilikamilika siku ya Jumatano wiki hii katika uwanja wa Kimataifa wa Michezo wa Moi Kasarani jijini Nairobi nchini Kenya. 

Katika fainali ya kwanza ya wasichana, Uganda ilitoka nyuma na kushinda mabao 2-1 dhidi ya Kenya waliokuwa waandalizi na washiriki kwa mara ya kwanza. Baadaye timu ya wavulana ya Uganda ilinyanyua ubingwa baada ya kuifunga Tanzania kupitia mikwaju ya penalti mabao 4-2 kufuatia sare ya bao 1-1 katika muda wa kawaida. 

Winga wa Kenya Faith Boke dhidi ya Lydia Namaseruka (9) na Mercy Namuhenga (aliyezibwa) wa Uganda
Winga wa Kenya Faith Boke dhidi ya Lydia Namaseruka (9) na Mercy Namuhenga (aliyezibwa) wa Uganda © FKF

Kwa upande wa wasichana, mabao ya Uganda yalitiwa kimiani na Shadia Nabirye dakika ya 18 na Shaluwah Butini sekunde chache baada ya kipindi cha pili kuanza na hivyo basi kuwahakikishia ubingwa baada ya kumaliza nafasi ya tatu kwenye mashindano ya kufuzu msimu jana. Kenya ilijiweka kifua mbele dakika ya saba kupitia Lindey Weey Atieno aliyefunga kwa njia ya mpira wa ikabu. 

Kocha wa Uganda, Moses Nkata alifichua siri ya Uganda kutamba katika siku za hivi karibuni haswa baada ya timu ya Uganda U18 kunyakua ubingwa dhidi ya Kenya wikendi iliyopita jijini Kisumu nchini Kenya 

Katika soka la wasichana, Kenya na Tanzania ziko mbele yetu na tulijaribu kuwaiga tangu awali ili kucheza soka nzuri. Matunda umeyaona. Mizizi yetu ya mashinani ni dhabiti.

Uganda ilifika fainali bila kupoteza mechi yoyote kwa kufungwa bao moja tu katika mechi tano. Kwenye makundi, Uganda ilitoa sare ya 0-0 dhidi ya Tanzania siku ya kwanza ya mashindano kabla ya kushinda mechi tatu mfululizo - Burundi 4-0, Rwanda 3-0 na Kenya 1-0. 

Waziri wa Michezo nchini Kenya Ababu Namwamba akipokeza tuzo timu ya kina dada ya Uganda
Waziri wa Michezo nchini Kenya Ababu Namwamba akipokeza tuzo timu ya kina dada ya Uganda © FKF

Kocha wa Kenya, Jackline Juma, alikuwa mwingi wa majuto baada ya fainali ya Jumatano. 

Mchezo ulikuwa mzuri, tulipata nafasi zetu ila hatukutumia nyingi. Katika soka usipotumia nafasi zako vizuri utaadhibiwa. Uganda ni timu nzuri lakini nawapongeza wasichana wangu.

Kwenye makundi, Kenya ilianza vizuri kwa kushinda mechi tatu (Rwanda 2-0, Tanzania 1-0, Burundi 2-0) kabla ya kupoteza 1-0 dhidi ya Uganda. 

“Timu nzima kwa ujumla ni timu nzuri ikizingatiwa ni mara yao ya kwanza kucheza michuano hii. Tutarejea mazoezini na kufanyia kazi mambo machache ili kurejea kama timu tofauti,” alisisitiza kocha Juma. 

Timu ya Kenya ya wasichana iliyomaliza nafasi ya pili kwenye mashindano
Timu ya Kenya ya wasichana iliyomaliza nafasi ya pili kwenye mashindano © FKF

Kwa upande wa wavulana, mchezaji wa Uganda Ashraf Kyakuwa aliifungia Uganda bao la kwanza dakika ya 34 kwa njia ya mpira wa ikabu. Dakika sita baadaye Alvin Hangu alisawazisha kwa shuti kali ndani ya kijisanduku kufuatia mkwaju wa faulo wa mchezaji Aivan Mashaka nje kidogo ya kijisanduku uliobabatiza ukuta wa binadamu wa Uganda.   

"Mchezo umekuwa mzuri, Uganda wamekuwa wapinzani wagumu lakini vijana wangu wamejikakamua sana hadi mikwaju ya penalti. Ninawapongeza sana," Elieneza Nicholas, kocha wa Tanzania. 

Uganda dhidi ya Tanzania kwenye mechi ya fainali ya wavulana uwanjani Kasarani
Uganda dhidi ya Tanzania kwenye mechi ya fainali ya wavulana uwanjani Kasarani © FKF

"Mchezo ulikuwa mgumu kidogo kwa sababu kucheza dhidi ya timu moja mara mbili si rahisi. Niliwaandaa vijana wangu kwa mchezo wa wazi na hatua ya penalti. Tunaenda kujiandaa kwa hatua inayofuata sasa," Daniel Abel, kocha wa Uganda. 

Washindi walijinyakulia $100,000, nafasi ya pili $750,000 na nafasi ya tatu $50,000. 

   ‘Chema chajiuza’ 

Kwa upande wa wasichana, tuzo ya fair play ilitunukiwa timu ya taifa ya Kenya huku Tanzania ikirejea nyumbani na medali ya shaba nayo Uganda medali ya dhahabu kama mabingwa. 

Mlinga lango Huda Ayikeru na mshambuliaji Shadia Nabirye wa Uganda walituzwa kipa bora na mfungaji bora (mabao matano) mtawalia. Mkenya Lindey Weey Atieno alitajwa kuwa mchezaji bora wa mashindano. 

Timu ya Tanzania ya wasichana iliyomaliza nafasi ya tatu mashindanoni
Timu ya Tanzania ya wasichana iliyomaliza nafasi ya tatu mashindanoni © FKF

Katika kitengo cha wavulana, tuzo ya fair play na medali ya shaba zilitunukiwa mwenyeji Kenya. Tanzania iliyomaliza nafasi ya pili ilituzwa medali ya fedha huku Uganda ikinyakua dhahabu kwa kutwaa taji hilo. 

Kipa Abraham Nassor kutoka Tanzania alishinda tuzo ya kipa bora huku mshambuliaji Simon Wanyama wa Uganda akitunukiwa mfungaji bora kwa kufunga mabao sita. Kyakuwa wa Uganda alizawadiwa tuzo ya mchezaji bora wa michuano hiyo. 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.