Pata taarifa kuu

DRC: Mkutano kati ya makundi yenye silaha na serikali kufanyika mwezi Januari

Makundi yenye silaha na serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo watafanya kikao kijacho cha mazungumzo ya amani mnamo mwezi wa Januari mashariki mwa DRC, baada ya mikutano mitatu ya awali nchini Kenya, Jumuiya ya Mataifa ya Afrika Mashariki (EAC), imetangaza Jumanne wiki hii.

Uhuru Kenyatta, Rais wa zamani wa Kenya na mwezeshaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, akihutubia wajumbe wanaosimamia mchakato wa amani katika eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, jijini Nairobi, Kenya, Desemba 5 2022.
Uhuru Kenyatta, Rais wa zamani wa Kenya na mwezeshaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, akihutubia wajumbe wanaosimamia mchakato wa amani katika eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, jijini Nairobi, Kenya, Desemba 5 2022. REUTERS - MONICAH MWANGI
Matangazo ya kibiashara

Tangazo hili limetolewa mwishoni mwa kikao cha tatu cha "mazungumzo kati ya wadau katika mazungumzo ya DRC", ambayo yalileta pamoja kwa siku nane mjini Nairobi wawakilishi wa takriban makundi hamsini yenye silaha, serikali na mashirika ya kiraia.

Kundi la waasi la M23, ambalo linaongoza mashambulizi mashariki mwa nchi hiyo na ambalo Kinshasa inalielezea kama kundi la "kigaidi", halishiriki katika mijadala hii.

"Kikao kitafanyika mwezi Januari mjini Goma na Bunia ili kutathmini maendeleo (yaliyopatikana) na kuanza kushughulikia ajenda ya muda wa kati na mrefu," EAC, ambayo ni mpatanishi wa mazungumzo hayo, imesema katika taarifa yake.

Washiriki pia walisisitiza makubaliano yao ya "kudumisha usitishaji vita pamoja na kuachiliwa kwa wanajeshi watoto na kupata misaada ya kibinadamu", linaongeza shirika hilo.

"Tumeridhika na hatua tuliyofikia. Hatusemi kwamba tumemaliza kila kitu, lakini tumepiga hatua fulani," amesema, bila maelezo zaidi, Rais wa zamani wa Kenya, Uhuru Kenyatta, ambaye anahudumu kama "mwezeshaji" wa mchakato wa Nairobi.

"Ninatumai kwamba tutakapokutana tena Goma - hii inapaswa kuwa kati ya mwezi wa Januari na Februari - tunaweza kuripoti maendeleo juu ya pointi ambazo tumekubaliana hapa," ameongeza.

Mkutano huu wa tatu unafanyika, huku Mashariki mwa DRC ikikumbwa na kuibuka tena kwa ghasia na mashambulizi ya M23, ambayo Kinshasa ilishutumu siku ya Jumatatu kwa kuwaua takriban raia 300 mwishoni mwa mwezi wa Novemba. Vita hivi ni mada ya mazungumzo tofauti, yaliyoandaliwa na Angola.

Waasi wa zamani wa Watutsi walioshindwa mwaka wa 2013, M23 walichukua tena silaha mwezi wa Novemba 2021 na katika miezi ya hivi karibuni wameteka sehemu kubwa ya eneo la kaskazini mwa Goma, mji mkuu wa mkoa wa Kivu Kaskazini. Mashambulizi ya hivi karibuni ya M23 yanachochea mvutano wa kidiplomasia kati ya DRC na Rwanda, zote wanachama wa EAC.

Kinshasa inaishutumu Rwanda kwa kutoa msaada kwa M23 ambao wataalamu wa Umoja wa Mataifa na maafisa wa Marekani pia walieleza katika miezi ya hivi karibuni. Kigali inazozana, ikiishutumu Kinshasa kwa kushirikiana na FDLR, waasi wa Kihutu wa Rwanda, kundi lililoanzishwa nchini DR Congo tangu mauaji ya halaiki ya Watutsi mwaka 1994 nchini Rwanda.

EAC imekuwa ikifanya kazi ya kuleta utulivu mashariki mwa DRC, ambayo imekuwa ikikumbwa na ghasia kutoka kwa zaidi ya makundi 100 yenye silaha kwa karibu miaka 30. Nchi saba wanachama wa EAC (Burundi, Kenya, Uganda, DRC, Rwanda, Sudan Kusini, Tanzania) ziliamua mwezi Juni kutuma kikosi cha kikanda ambacho kimeanza kuwasili kwenye ardhi ya DRC.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.