Pata taarifa kuu
HAKI-SHERIA

Waandishi watatu wa Uganda wafutwa kazi kwa kufanya mzaha kuhusu bunge

Wafanyakazi watatu wa televisheni moja ya kibinafsi nchini Uganda wamefutwa kazi baada ya kukejeli kura iliyopigwa bungeni katika matangazo yaliyorushwa hewani, kituo hicho kimetangaza siku ya Ijumaa, huku kikiomba radhi.

Moja ya vikao vya Bunge la Uganda mnamo mwaka 2017.
Moja ya vikao vya Bunge la Uganda mnamo mwaka 2017. © Ronald Kabuubi/AP
Matangazo ya kibiashara

Kituo cha televisheni cha kibinafsi Baba TV kimesema kilipokea malalamishi dhidi ya mtangazaji Simon Muyanga Lutaaya, ambaye Jumanne alitania kuhusu onyo rasmi lililopigiwa kura na wabunge dhidi ya Waziri wa Makazi Persis Namuganza.

"Nataka kulishukuru Bunge, matatizo ya Uganda hatimaye yametatuliwa (kwa uamuzi huu). Hospitali zitakuwa na dawa, barabara zetu zitakuwa sawa, vijana watapata ajira," alisema.

Waandishi wengine wawili wa habari walioandamana na Simon Muyanga Lutaaya kwa matangazo hayo pia wamechukuliwa hatua ya kufutwa kazi. Baba TV, yenye makao yake makuu katika mji mkuu Kampala, imesema siku ya Ijumaa kuwa baadhi ya wabunge pamoja na maafisa kutoka Tume ya Mawasiliano ya Uganda (UCC), shirika linalodhibiti vyombo vya habari, wamelalamikia matamshi hayo.

"Walalamikaji waliona picha hizo kama za kufedhehesha, kudhihaki na kukejeli taasisi ya bunge, viongozi wake na waheshimiwa wabunge," Baba TV imesema katika taarifa yake.

"Kama kituo kinachojitolea na kuwajibika kwa watazamaji wake, menejimenti imechukua hatua za ndani kuzuia hili kutokea katika siku zijazo, ikiwa ni pamoja na kusimamishwa kwa timu nzima ya wanahabari hao," Baba TV imesema huku ikiendelea kuomba radhi kwa Bunge na UCC.

Bw. Lutaaya na wanahabari wengine wawili pia waliomba radhi Bunge na UCC. Mpinzani Bobi Wine alikosoa kufutwa kazi kwa wafanyakazi hao, akiliambia shiika la habari la AFP kwamba hatua inayotakiwa na chama tawala inadhihirisha "ukosefu wa haki na kijeshi ambao lazima upigwe vita na Waganda wote wenye uwezo".

Uganda, nchi ya Kiafrika katika eneo la Maziwa Makuu inayotawaliwa kwa mkono wa chuma tangu 1986 na Yoweri Museveni, inashika nafasi ya 132 (kati ya 180) katika orodha ya dunia ya uhuru wa vyombo vya habari ya mwaka 2022 iliyotolewa na shirika lisilo la kiserikali linalotetea waandishi wa habari wasio na mipaka, RSF.

RSF inaamini kwamba 'waandishi wa habari wanakabiliwa na vitisho na vurugu karibu kila siku'.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.