Pata taarifa kuu

Kenya: Mvua kubwa yasababisha vifo Nairobi

Watu kumi wamefariki na wengine kadhaa hawajulikani waliko siku ya Jumatano katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, ambapo vitongoji vimekumbwa na mafuriko baada ya mvua kubwa kunyesha kunyesha usiku wa Jumanne kuamkia Jumatano, kulingana na shirika la habari la AFP likinuku polisi.

Mvua zisizo za kawaida za mwaka huu katika Afrika Mashariki zimechochewa na mfumo wa hali ya hewa iitwayo El Niño.
Mvua zisizo za kawaida za mwaka huu katika Afrika Mashariki zimechochewa na mfumo wa hali ya hewa iitwayo El Niño. © AFP
Matangazo ya kibiashara

Jumla ya "watu 60,000, hasa wanawake na watoto", "waliathiriwa pakubwa na mafuriko ya ghafla na mabaya ambayo yalikumba jiji hilo", akulingana na polisi ya kenya katika taarifa yake, ikithibitisha kwamba Nairobi "iko ukingoni mwa janga la kibinadamu. Kupanda kwa maji kumeathiri vitongoji vya watu wenye maisha duni vyote viwili, kama vile Mathare, na vitongoji vingine vya watu wa hali ya juu, kama vile Runda ambapo makao makuu ya kanda ya Umoja wa Mataifa yanapatikana.

Kenya inaendelea kukumbwa na mvua kubwa inayonyesha Afrika Mashariki, ambapo msimu wa mvua unazidishwa na mfumo wa  hali ya hewa unaoitwa El Niño. Shirika la Umoja wa Mataifa la kutoa misaada ya kibinadamu (OCHA) liliripoti, kufikia Aprili 18, takriban watu 32 walifariki dunia na zaidi ya 40,000 kuhama makazi yao katika kaunti 21 kati ya 47 za nchi hiyo tangu kuanza kwa msimu wa mvua mwezi Machi.

Jijini Nairobi, mvua kubwa iliyonyesha usiku kucha ilisababisha mito ya Athi, Ngong na Mau Mau kuvunja kingo zake. Katika kitongoji cha watu wenye maisha duni cha Mathare, mojawapo ya maeneo yaliyoathirika zaidi, wakaazi walimezwa na maji hadi kiunoni, kulingana na picha zilizotolewa na Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya ambalo lilikuwa likifanya shughuli za kuwahamisha kutoka eneo hilo.

Picha nyingine zilizotumwa kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha watu wakiwa wamekimbilia kwenye paa za bati za nyumba zao. Barabara zimejaa maji, huku baadhi ya mitaa iliyo Mashariki mwa jiji hilo, ikifurika na kusababisha wakaazi kushindwa kuingia wala kuondoka. Katika kituo cha biashara (CBD), mojawapo ya njia kuu ilizibwa Jumatano asubuhi kwa kuanguka kwa miti miwili iliyong'olewa na kuangukia barabarani.

Shirika la reli nchini Kenya Railways limetangaza kusitiisha usafiri wa treni za abiria, "kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha iliyoathiri njia".

Seneta Edwin Sifuna, mmoja wa viongozi wa upinzani amesema kwenye mtandao wa X kwamba hali ya Nairobi "imefikia viwango vya juu" na kwamba mamlaka za kaunti "zimezidiwa." "Tunahitaji (kuona) huduma zote za dharura za kitaifa zikihamasishwa kuokoa maisha ya watu," aliongeza.

Takriban kilomita kumi na tano kaskazini mwa mji mkuu, katika kaunti jirani ya Kiambu, wakazi wenye hasira walifunga barabara kuomba mamlaka kuwasaidia. Walitawanywa kwa mabomu ya machozi. Siku ya Jumanne, polisi wa Kenya walitangaza kuwa wamemuokoa mtoto wa miaka mitano kwa kutumia helikopta, aliyenaswa kwa siku kadhaa kutokana na kupanda kwa maji katika kaunti ya Machakos, takriban kilomita 150 mashariki mwa mji mkuu.

Nchi kadhaa za mashariki mwa Afrika zimeathiriwa katika wiki za hivi karibuni na kiwango kisicho cha kawaida cha mvua, kilichosababishwa haswa na mfumo wa hali ya hewa iitwayo El Niño iliyoanza katikati ya mwaka 2023 na inaweza kudumu hadi mwezi Mei, shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) ilionya mnamo mwezi Machi. Nchini Tanzania, takriban watu 58 walifariki kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha na makumi ya maelfu kuyahama makazi yao katika wiki mbili za kwanza za mwezi wa Aprili. Nchini Burundi, mamlaka imeripoti wakimbizi wa ndani 96,000 kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha kwa miezi kadhaa.

Eneo hilo tayari limekumbwa na uharibifu mkubwa wa El Niño, chanzo cha mvua kubwa. Mwezi Desemba, zaidi ya watu 300 walifariki katika majanga mbalimbali yaliyosababishwa na mvua kubwa nchini Kenya, Ethiopia na Somalia. Kuanzia mwezi Oktoba 1997 hadi Januari 1998, mafuriko makubwa yaliyochochewa na mvua kubwa iliyosababishwa na El Niño yalisababisha vifo vya zaidi ya watu 6,000 katika nchi tano katika eneo hilo.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.