Pata taarifa kuu
AFCON 2023

Cote D'Ivoire kumkosa mshambuliaji Sébastien Haller dhidi ya Guinea Bissau

Abidjan, Cote D'Ivoire – Ni saa chache zimesalia kabla ya kipenga cha kwanza cha Kombe la Mataifa ya Afrika ya mwaka 2023 kuanza nchini Cote D’Ivoire. Wenyeji Ivory Coast watapambana na Guinea Bissau katika uwanja wa Alassane Ouattara D’Ebimpe jijini Abidjan Jumamosi hii. Timu hizo zimefanya kikao na wanahabari leo mchana.

Kocha wa Cote D'Ivoire Jean-Louis Gasset na kiungo Frenkie Kessie kwenye kikao cha wanahabari 12/01/2024
Kocha wa Cote D'Ivoire Jean-Louis Gasset na kiungo Frenkie Kessie kwenye kikao cha wanahabari 12/01/2024 © Jason Sagini
Matangazo ya kibiashara

Kocha wa Cote D’Ivoire Jean-Louis Gasset amefichua kuwa mshambuliaji wa Borussia Dortmund ya Ujerumani, Sébastien Haller na winga wa Brighton ya Uingereza Simon Adingra hawatakuwepo kwenye kikosi kwa mechi ya kwanza.

Kati ya mechi ya kwanza na ya pili, kuna siku tano. Tumewafanyia vipimo vya MRI, tutaona tarehe za mwisho. Nina malengo makubwa sana kwa Sébastien Haller na Simon Adingra

Haller na Adingra wangali wanauguza majeraha waliyopata wakichezea vilabu vyao.

Ivory Coast wamekuwa mazoezini wiki nzima jijini San Pedro kabla ya kurejea kwenye makaazi yao jijini Abidjan.

Tumejiandaa vizuri. Nimegundua kuna shinikizo kubwa ya hamu ya kushinda taji. Swali ni jinsi ya kudhibiti shinikizo. Tunajua timu zinazopigiwa upato mkubwa. Kuna bingwa mtetezi, kuna aliyefika nusu fainali ya Kombe la Dunia. Lakini tuna njia zetu ila pia tunawaheshimu wapinzani wetu sana.

Hii ni mara ya pili Cote D’Ivoire kuandaa mashindano haya makubwa barani Afrika baada ya kuandaa mwaka 1984. ‘Wanatembo’ hao ni mabingwa mara mbili (1992 na 2015).

Kiungo wa Ivory Coast, Frenkie Kessie ameahidi kufanya vizuri kwenye mechi ya kwanza na hata kwenye mashindano yote kwa kuwarai mashabiki wa nyumbani kujitokeza kwa wingi.

Kucheza AFCON nyumbani ina maana kubwa. Tunasikiliza maagizo ya kocha. Tuko tayari kuweka historia nyumbani. Mashabiki wa nyumbani lazima wawe mtu wa kumi na mbili, wajitokeze kwa wingi kutuunga mkono

Kocha wa Guinea Bissau Baciro Cande amesifia uteuzi wa kikosi chake akiamini wana uwezo mkubwa wa kutoa ushindi katika mechi ya kwanza.

Wachezaji wetu ni wa kiwango cha juu na wamezoea kushiriki katika mashindano ya kimataifa. Ivory Coast ni taifa kubwa.

Guinea Bissau inashiriki mashindano haya kwa mara ya nne ambapo haijawahi kufuzu hatua ya mtoano.

Tuna mipaka kuhusu maandalizi. Tumekuwa tukijiandaa kwa wiki moja. Tutacheza kama kawaida tu

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.