Pata taarifa kuu
AFCON 2023

Adel Amrouche: Hamna nafasi ya makosa kujirudia tena dhidi ya Zambia na DRC

San Pedro, Cote d'Ivoire – Kocha wa timu ya taifa ya Tanzania, Adel Amrouche amekariri kuwa hataruhusu makosa kujirudia kuelekea mechi ya pili ya makudi kwenye Kombe la Mataifa ya Afrika baada ya kupoteza 3-0 dhidi ya Morocco katika mechi ya ufunguzi siku ya Jumatano uwanjani Laurent Pokou jijini San Pedro nchini Cote d’Ivoire.

Kocha wa Tanzania, Adel Amrouche kwenye kikao na wanahabari ya mechi dhidi ya Morocco 17/01/2024
Kocha wa Tanzania, Adel Amrouche kwenye kikao na wanahabari ya mechi dhidi ya Morocco 17/01/2024 © Jason Sagini
Matangazo ya kibiashara

Morocco ilijiweka kifua mbele dakika ya thelathini kupitia beki Roman Saiss baada ya mkwaju kali wa ikabu aliouchonga winga Hakim Ziyech. Iliichukua Simba hao wa jagwani dakika nne tu kupata magoli zaidi kipindi cha pili.

"Bado tuna mechi mbili. Tutajaribu kurekebisha yaliyotokea leo. Tuko kwenye mojawapo ya makundi magumu kweli na najua wachezaji wanafahamu hilo. Natumai kwa mechi zijazo hatutarudia makosa ya kupoteza umakini mchezoni".

Mshambuliaji wa Morocco Youssef En-Neysri akisherehekea baada ya kufunga bao
Mshambuliaji wa Morocco Youssef En-Neysri akisherehekea baada ya kufunga bao © CAF

Nahodha wa Tanzania, Ally Mbwana Samatta alikiri ugumu wa mechi hiyo.

"Morocco walikuwa bora, inabidi tukubali. Tulijaribu kucheza kwa nidhamu na kufuata maelekezo ya walimu. Unapocheza na mpizani kama Morocco na akakutangulia na wana wachezaji ambao wanaweza kumiliki mpira kwa muda mrefu, inakuwa vigumu kupata nafasi ya kutengeneza goli,".

Samatta anaendelea kusema “inabidi waweke hisia pembeni kwa ajili ya kufanya vizuri kwa mechi zinazokuja.”

Kiungo Azzedine Ounahi wa Morocco ambaye alifunga bao moja alitajwa mchezaji bora wa mechi hiyo.

Tanzania ilimaliza mchezo na wachezaji kumi uwanjani baada ya beki wa winga Novatus Miroshi kuoneshwa kadi nyekundu. 

Kocha wa Morocco Walid Regragui alisema wako tayari kupambana na timu yoyote kwenye mashindano. Morocco ni mojawapo ya timu zinazopigiwa upato mkubwa kushinda kombe hilo.

"Tuko kwenye misheni hapa. Kila mtu anataka kucheza na sisi na tuko tayari," amesema kocha Regragui.

DRC, Zambia nguvu Sawa

Mabingwa mara mbili DRC walitoshana na nguvu na mabingwa wa mwaka 2012 Chipolopolo ya Zambia katika mechi iliyofuata uwanjani humo

DRC ilianza mechi kwa kasi ya juu kwa mfululizo wa mashambulizi ila dakika ya 23, Kings Kangwa wa Zambia akaipatia Zambia uongozi. Mlinga lango wa Leopard Lionel Mpasi alitoka kwenye lango lake kuzuia shambulizi la kushtukiza ila akachezewa visivyo na mpira ukatoka nje.

Kings Kangwa wa Zambia baada ya kuipatia Chipolopolo bao la kuongoza dhidi ya DRC
Kings Kangwa wa Zambia baada ya kuipatia Chipolopolo bao la kuongoza dhidi ya DRC © CAF

Mlinga lango wa Leopard Lionel Mpasi alitoka kwenye lango lake kuzuia shambulizi la kushtukiza ila akachezewa visivyo na mpira ukatoka nje.

Mpasi alidhani mwamuzi Bamlak Tessema kutoka Ethiopia ataashiria mpira wa adhabu ila akaashiria mpira wa kurusha. Patson Daka alimrushia Kings ambaye alichonga mpira mrefu kutumbukia kwenye wavu kabla ya golikipa kurudi langoni pake.

Hata hivyo, uongozi huo haukudumu kwa muda mrefu kwani DRC ilifanya shambulizi la haraka dakika nne baadaye pale ambapo Gael Kakuta alimpakulia mpira mrefu Cedric Bakambu kutoka katikati ya uwanja na kuandaa krosi ya chini chini aliyounganisha wavuni mshambuliaji Yoanne Wissa ambaye alitajwa mchezaji bora wa mechi

Kocha wa DRC, Sébastien Desabre anaamini walijilinda vyema dhidi ya Zambia lakini pia walijifunza mengi kutoka kwa mchezo huo.

"Tunastahili kujinoa kwenye ushambuliaji, tulikuwa na nafasi nyingi sana na tulistahili ushindi. Zambia wanajua kuzuia vizuri pia," amesema.

Mshambuliaji wa klabu ya Brentford ya Uingereza, Yoanne Wissa ambaye alifunga bao alichaguliwa kama mchezaji bora wa mechi.

"Nafurahia kufunga bao licha ya kuwa haikutuwezesha kushinda. Natumai Jumapili mambo yatakuwa bora na utakuwa mchezo tofauti kabisa," ameeleza.

Yoanne Wissa (DRC) - mchezaji bora wa mechi dhidi ya Zambia
Yoanne Wissa (DRC) - mchezaji bora wa mechi dhidi ya Zambia © Jason Sagini

Baada ya raundi ya kwanza, Morocco inaongoza kundi F kwa alama tatu ikifuatwa na DRC na Zambia kwa alama moja kila mmoja mtawalia kisha Tanzaniia ya mwisho bila alama yoyote.

Timu hizi nne zitacheza mechi ya pili ya makundi kila mmoja Jumapili wikendi hii katika uwanja uo huo wa Laurent Pokou.

Ratiba (Jumapili):

Morocco vs DR Congo

Zambia vs Tanzania

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.