Pata taarifa kuu
AFCON 2023

Morocco, DRC, Tanzania, Zambia tayari kupambana raundi ya pili hatua ya makundi

San Pedro, Cote d'Ivoire – Jumamosi wikendi hii, makocha na wachezaji wa timu zinazoshiriki kundi F kwenye Kombe la Mataifa ya Afrika walizungumza kabla ya mechi za raundi ya pili kuchezwa Jumapili jioni. Tanzania itakutana na Zambia nayo DRC ipambane na Morocco katika uwanja wa Laurent Pokou jijini San Pedro.

Hemed Suleiman (kushoto) na Juma Mgunda (kulia) kwenye mazoezi ya Taifa Stars jijini San Pedro
Hemed Suleiman (kushoto) na Juma Mgunda (kulia) kwenye mazoezi ya Taifa Stars jijini San Pedro Β© TFF
Matangazo ya kibiashara

Kaimu kocha wa Tanzania Hemed Morocco amesema hana shinikizo yoyote kujaza nafasi ya kocha mkuu kufuatia marufuku ya kocha mkuu Adel Amrouche na CAF, kufuatia matamshi aliyotoa kuhusu Morocco kwenye soka a Afrika.

Hemed amesisitiza β€œkocha wetu hajafukuzwa, ni kupigwa marufuku tu na yeye bado ni kocha wetu."

Sina presha yoyote. Ni jukumu kubwa kujaza hii nafasi lakini nitajitahidi zaidi. Mimi si mgeni katika haya mashindano. Mara nyingi hutokea kocha anapooneshwa kadi nyekundu pia. Tutatumia mbinu na mipango ile ile ambayo kocha alikuwa ameweka.

Hemed, amethibitisha hali shwari ya wachezaji wote kambini kuelekea mechi hiyo muhimu, akidai kisaikolojia wako sawa kabisa na hawana majeruhi yoyote.

Tunajua Zambia ni timu nzuri, tunawaheshimu. Tulipoteza mechi ya kwanza wao walipata sare. Tumesuluhisha makosa kadhaa kwenye mazoezi kutoka kwa mchezo dhidi ya Morocco.

Kiungo wa Taifa Stars, Himid Mao amesema wana timu changa ambayo itatamba miaka ijayo.

Hatuwezi kuahidi chochote, naahidi tu kujituma na kuzalisha matokeo ya kuridhisha.Tuko tayari kupambana na Zambia.

Ni kauli ambayo mchezaji wa Zambia, Fashion Sakala ameshikilia kuhusu timu yao.

Wengi wetu haya ni mashindano yetu ya kwanza na tunajaribu kutiana moyo. Tulicheza vizuri kwenye mechi za kufuzu na hata kupata sare dhidi ya DRC haikuwa rahisi. Tuko tayari kupambana na Tanzania.

Kocha mkuu wa Zambia Avram Grant, alitaja umuhimu wa kupata matokeo mazuri baada ya Chipolopolo kurejea mashindanoni baada ya muda mrefu (tangu 2015) na kupata sare mechi ya kwanza.

Nilifurahi baada ya mechi ya kwanza ila mechi ya pili ni muhimu sana kwetu, tunataka kufuzu hatua ya mtoano.

Chui na Simba Jangwani!

Kocha wa DRC, Sebastian Desabre amesema mechi yao dhidi ya Morocco itakuwa fainali ya pili mashindanoni huku wakilenga ushindi.

Naifahamu Morocco vizuri. Nina ufahamu wa wachezaji kadhaa wenye uzoefu mkubwa lakini si kizuizi kwetu sababu hiyo itatusukuma kufanya vizuri zaidi.

Desabre amesisitiza haja ya kuepuka makosa waliyofanya kwenye sare ya 1-1 dhidi ya Zambia kwa kucheza kwa kasi na kusoma mbinu za Morocco uwanjani mapema.

Kocha Desabre aligusia uwezo wa mshambuliaji Fiston Mayele na uwezekano wa kuanza mechi huku akidai anaonesha viwango vya juu na huenda wakalifikiria kabla ya kuchagua kikosi cha kwanza. Mayele alikaa kwenye benchi muda wote katika mechi dhidi ya Zambia.

Kuhusu lengo la timu ya Leopard kwenye haya mashindano, kocha Desabre alisema nia yao si kushinda taji bali kujenga timu bora ambayo itashinda mataji katika mashindano yajayo.

Kwa upande mwingine, kocha wa Morocco Walid Regragui ameonesha heshima kubwa kwa timu ya DRC.

Tunawaheshimu ila hatuwaogopi. Wana wachezaji wazuri na lazima tuzingatie hilo. Haitakuwa mechi rahisi kama jinsi wengi wanavyodani.

Walid ameendelea kusema wanatafuta alama zote tatu katika mechi hiyo ila wataridhika na sare huku akitaja mbinu na mfumo wa kucheza mchezo huo kama kigezo cha msingi kabisa.

Wachezaji wa Morocco kwenye mazoezi
Wachezaji wa Morocco kwenye mazoezi Β© Γ‰quipe du Maroc

Wachezaji wetu wote wako katika hali nzuri. Tunafanya uchambuzi kwa mpinzani yeyote tunayekwenda kukutana naye. Tunahitaji kuwa jasiri ili kushinda kila mechi.

Hata hivyo, kocha Regragui ametaja mapendeleo yao ya kucheza usiku tofauti na mechi hii iliyopangwa kuchezwa mchana.

β€œWachezaji wetu ni wa kitaalamu kwa hivyo wanapaswa kubadilika kuendana na mazingira.”

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.