Pata taarifa kuu
AFCON 2023

Tanzania yamsimamisha kazi kocha Adel Amrouche baada ya marufuku ya CAF

San Pedro, Cote d'Ivoire – Tanzania imemsimamisha kazi kocha mkuu Adel Amrouche baada ya marufuku ya mechi nane na kupigwa faini ya $10,000 na Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF).

Kocha Adel Amrouche kwenye mahojiano ya wanahabari kwenye AFCON 2023 jijini San Pedro
Kocha Adel Amrouche kwenye mahojiano ya wanahabari kwenye AFCON 2023 jijini San Pedro © CAF
Matangazo ya kibiashara

CAF ilifikia uamuzi wa dhabu hiyo baada ya Shirikisho la Soka la Morocco (FRMF) kuwasilisha malalamishi kwa kamati ya nidhamu ya CAF kufuatia matamshi yaliyotolewa na Amrouche, wakidai kukiuka kanuni za maadili.

Muktadha:

CAF ilisema "imemsimamisha kazi kocha huyo kwa mechi nane baada ya matamshi aliyoyatoa kuhusu maafisa wa Morocco kwenye mahojiano na runinga moja."

"Shirikisho la Morocco ni nguvu iliyothibitishwa katika ulimwengu wa soka ya Afrika. Morocco inasimamia soka ya Afrika," Amrouche aliiambia runinga moja nchini Algeria katika mahojiano kabla ya Kombe la Mataifa 2023 kuanza nchini Ivory Coast.

Amrouche mzaliwa wa Algeria alidai maafisa wa Morocco ndani ya CAF huamua ni nani waamuzi wa mechi zinazohusisha timu ya taifa ya wanaume ya Morocco, na muda wa mechi kuanza.

Tulitaka kucheza mechi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia dhidi ya Morocco Novemba mwaka jana mchana, lakini CAF ilipanga mechi hiyo jioni.

Kocha huyo aliamini kuwa mechi ya alasiri katika joto kali la Dar es Salaam ingependelea Tanzania, kwa kuwa wachezaji wengi wa Morocco watakuwa wakitokea katika vilabu vya Ulaya msimu wa baridi.

Nchi hizo mbili zilikutana siku ya Jumatano wiki jana, katika Kundi F kwenye mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika 2023, huku Morocco ikishinda 3-0.

Taarifa ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imesema imemsimamisha kazi Amrouche baada ya kauli ya kocha huyo.

Siku ya Jumanne, Rais wa TFF Wallace Karia alilitenga shirikisho hilo na kauli za Amrouche.

"Sisi kama TFF hatukubaliani na maoni yake," Karia alisema kwenye video iliyochapishwa na Azam TV.

Hizo ni hisia zake binafsi kama kocha, sisi ni wanachama wa CAF, na tunajua CAF inafuata taratibu zake bila ushawishi wa nchi yoyote. TFF na shirikisho la soka la Morocco ni marafiki.

Amrouche alitoa maoni yake kabla ya mechi yao ya ufunguzi ya Afcon 2023 dhidi ya Simba hao wa jangwani.

Nilizungumza mwezi mmoja uliopita, nikisema ni moja ya timu bora zaidi duniani. Walifika nusu fainali ya Kombe la Dunia. Sio timu inayoshinda kwa bahati, wanashinda kwa uwezo wao. Wanastahili.

Naibu kucha Hemed Suleiman Ali ameteuliwa kuinoa Taifa Stars kwa muda akisaidiwa na Juma Mgunda.

Hemed Suleiman (kushoto) na Juma Mgunda (kulia) kwenye mazoezi ya Taifa Stars jijini San Pedro
Hemed Suleiman (kushoto) na Juma Mgunda (kulia) kwenye mazoezi ya Taifa Stars jijini San Pedro © TFF

Tanzania inajaribu kutinga hatua ya mtoano kwa mara ya kwanza ikiwa ni mara ya tatu kushiriki michuano ya Afcon.

Amrouche aliteuliwa kuwa mwalimu wa Tanzania mwezi Machi 2023, akiwaongoza kufuzu Afcon kwa kupata pointi moja dhidi ya taifa lake la kuzaliwa (Algeria) katika mechi yao ya mwisho ya kufuzu.

Kocha huyo mwenye umri wa miaka 55 amewahi kuzifunza timu za taifa za Equatorial Guinea, Burundi, Kenya, Libya na Botswana.

Tanzania itacheza na Zambia Jumapili hii kabla ya kuchuana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo siku ya Jumatano wiki ijayo.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.