Pata taarifa kuu
UGIRIKI-EU-DENI

Masoko ya dunia yatetereka baada ya Ugiriki kutangaza kufunga benki zake

Masoko ya dunia hii leo yamejikuta kwenye hali tete wakati huu nchi ya Ugiriki ikiwa imetangaza kuzifunga benki zake zote kwa muda wa juma moja na kuweka kiwango cha wananchi kutoa fedha kwenye mashine za ATM.

Wananchi wa Ugiriki wakiwa kwenye foleni wakisubiri kutoa fedha kwenye moja ya mashine za ATM.
Wananchi wa Ugiriki wakiwa kwenye foleni wakisubiri kutoa fedha kwenye moja ya mashine za ATM. (©Reuters)
Matangazo ya kibiashara

Hii leo wananchi wa Ugiriki wameamka wakiwa hawajui nini chakufanya kufuatia tangazo hili la Serikali linalonega kunusuru benki zake na uchumi wake wakati huu mazungumzo na wakopeshaji wa kimataifa yakiendelea kusuasua.

Lakini licha ya hali ngumu ya kifedha inayoikabili nchini ya Ugiriki, wakopeshaji wa kimataifa bado hawajafunga milango yao kwa taifa hilo kurejea kwenye meza ya mazungumzo kujaribu kuwashawishi wakopeshaji hao watoe fedha zaidi.

Kuvunjika kwa mazungumzo ya juma lililopita kati ya utawala wa Athens, wakopeshaji wa kimataifa na viongozi wa Umoja wa Ulaya, kumeibua maswali mengi kuhusu mustakabali wa taifa la Ugiriki kuendelea kusalia kwenye jumuiya ya Ulaya.

Masoko ya hisa duniani yameshuhudia kushuka kwa mauzo yao, ambapo soko la hisa kwenye nchi za Ufaransa, na Ujerumani yameshuhudia kushuka kwa mauzo yao kwa asilimia 4 saa chache baada ya masoko ya bara Asia nayo kushuhudia kushuka kwa thamani yao na hofu ya Ugiriki kujitoa kwenye Umoja wa Ulaya.

Serikali ya Ugiriki imetangaza kuweka ukomo kwa wananchi kutoa fedha kwenye mashine za ATM kuanzia leo mpaka July 6 mwaka huu, ambapo sasa mwananchi ataruhusiwa kutoa kiasi kisichozidi Euro 60 kwa siku, huku watalii wa kigini na taasisi nyingine muhimu zikiruhusiwa wakiruhusiwa kutoa zaidi.

Waziri mkuu wa Ugiriki, Alexis Tsipras amewataka wananchi kuwa watulivu wakati huu mashine nyingi za ATM zikiwa hazina fedha, huku masoko ya hisa nchi nzima yakitangaza kufunga huduma hizo hadi July 7 kwa mujibu wa tangazo la Serikali.

Katika hatua nyingine, waziri mkuu, Tsipras ametangaza kuwa nchi yake itaitisha kura ya maoni July 5 mwaka huu, kuamua iwapo nchi yao isalie kwenye Umoja wa Ulaya ama ijitoe kutokana na kutoelewana na wakopeshaji wake.

Wachambuzi wa mambo wanaona kuwa viongozi wengi wa Ulaya wanataka kuona Serikali ya waziri mkuu Tsipras inashindwa kujiendesha na kulazimika kuitisha uchaguzi mkuu wa mapema kujaribu kuurejesha utawala uliokuwa unafuata masharti ya wakopeshaji.

Rais wa Ufaransa, Francois Hollande akizungumzia mzozo unaoendelea nchini Ugiriki, amesema kuwa nchi hiyo iko huru kujitoa kwenye Umoja huo, na kwamba ni suala la Demokrasia kwa nchi yoyote mwanachama wa Umoja huo kuitisha kura ya maoni kuamua hatma yao kwenye jumuiya hiyo.

Rais Hollande ameongeza kuwa viongozi wa Athens, bado wanayo nafasi nyingine kujaribu kunusuru uchumi wake kwa kukubali kurejea kwenye mazungumzo ili kusaka suluhu.

Hatua hii ya Ugiriki imekuja saa chache baada ya benki ya Ulaya kutangaza kusitisha utoaji wa fedha za dharura kuisaidia Ugiriki.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.