Pata taarifa kuu

Tetemeko la ardhi Japani: Idadi ya vifo yaongezeka hadi 161, 103 hawajulikani walipo

Tetemeko kubwa la ardhi lililotikisa katikati mwa Japani mnamo Januari 1 lilisababisha vifo vya watu 161, wakati watu 103 bado hawajulikani walipo, kulingana na hesabu mpya iliyotangazwa Jumatatu asubuhi na viongozi wa eneo hilo.

Theluji inanyesha wakati waokoaji wakifanya shughuli ya utafutaji kuzunguka soko lililoteketea huko Wajima, wilaya ya Ishikawa, Japani Jumapili, Januari 7, 2024. Tetemeko kubwa la ardhi lilikumba Japani magharibi mnamo Januari 1, na kuua watu wengi, kuangusha majengo na kusababisha maporomoko ya ardhi.
Theluji inanyesha wakati waokoaji wakifanya shughuli ya utafutaji kuzunguka soko lililoteketea huko Wajima, wilaya ya Ishikawa, Japani Jumapili, Januari 7, 2024. Tetemeko kubwa la ardhi lilikumba Japani magharibi mnamo Januari 1, na kuua watu wengi, kuangusha majengo na kusababisha maporomoko ya ardhi. AP
Matangazo ya kibiashara

Tetemeko hilo la ardhi lenye ukubwa wa 7.5 kwenye kipimo cha Richter pia lilisababisha watu 560 kujeruhiwa, kwa mujibu wa taarifa kutoka eneo la Ishikawa, ambalo ndilo lililoathiriwa zaidi na maafa hayo.

Tetemeko hilo la ardhi, lililofuatwa na mamia ya mitetemeko ya baadaye, lilisababisha kuporomoka kwa majengo na barabara, na pia lilisababisha Tsunami, mawimbi ya urefu wa zaidi ya mita yakigonga kwenye ufuo wa rasi ya Noto, ukanda mwembamba wa ardhi wenye urefu wa kilomita mia moja unaosambaa ndani Bahari ya Japan.

Tetemeko hilo lilisikika hadi Tokyo, umbali wa kilomita 300.

Maelfu ya waokoaji kutoka kote nchini Japani, ambao wanaendelea kuchunguza vifusi wakitafuta miili, lazima wakabiliane na theluji iliyoanguka kwenye rasi ya Noto siku ya Jumatatu.

Maporomoko mapya ya ardhi kutokana na mvua yanahofiwa na hali ya barafu inatarajiwa kutatiza zaidi shughuli kwenye barabara zilizoharibiwa na tetemeko hilo, mamlaka imeonya.

- Barabara zilizoharibika -

Mtu mkongwe mwenye umri wa miaka 90 aliweza kutolewa akiwa hai kutoka kwenye vifusi siku ya Jumamosi baada ya kukaa kwa siku tano chini ya vifusi vya nyumba yake iliyoporomoka huko Suzu, kwenye ncha ya rasi hiyo.

Aliweza kujibu maswali kwa ufasaha alipookolewa na kupelekwa hospitalini kwa matibabu, shirika la utangazaji la NHK lilisema. “Subiri!” waokoaji walimfokea kwenye mvua, katika video iliyonaswa na polisi na kutangazwa na vyombo vya habari vya ndani. "Kila kitu kitakuwa sawa!", "Kaa sawa".

Wengi hawakubahatika: Katika mji wa Anamizu, pia kwenye rasi hiyo, mwanamume mwenye umri wa miaka 52 aliyepata habari kuhusu vifo vya mwanawe wa kiume mwenye umri wa miaka 21 na wakwe zake alikuwa akingoja habari za wanafamilia wengine.

"Nataka wawe hai. Ni jambo lisilofikirika kuwa nimeachwa peke yangu," ameliiambia shirika la habari la NHK.

Huduma za uokoaji pia zinaendelea na juhudi za kuwafikia watu waliotengwa kutokana na barabara kuharibiwa na tetemeko la ardhi, na kuwafikishia chakula na vifaa.

Takriban watu 29,000 walipewa hifadhi katika makazi 404 ya serikali siku ya Jumapili, kulingana na idara ya Ishikawa.

Tetemeko hili la ardhi ni la kwanza kusababisha vifo vya zaidi ya watu 100 nchini Japan tangu kutokea kwa tetemeko kubwa la ardhi huko Kumamoto (kusini-magharibi) na kusababisha vifo vya watu 276 mnamo mwaka 2016.

Japani ambayo ipo kwenye Gonga la Moto la Pasifiki, ni mojawapo ya nchi zilizo na matetemeko la ardhi la mara kwa mara.

Visiwa hivyo vimeandamwa na kumbukumbu ya tetemeko la ardhi la ukubwa wa 9.0 kwenye kipimo cha Richter lililofuatiwa na tsunami kubwa mnamo mwezi Machi 2011 kwenye pwani yake ya kaskazini mashariki, janga ambalo lilisababisha vifo vya watu 20,000 ikiwa ni pamoja na watu waliotoweka.

tetemeko hili a pia lilisababisha ajali ya nyuklia ya Fukushima, mbaya zaidi tangu Chernobyl mnamo mwaka 1986.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.