Pata taarifa kuu
UCHAGUZI-SIASA

'Ni wajibu wetu kupiga kura': India yaanza kupiga kura kwa ajili ya uchaguzi mkuu

Kuanzia Ijumaa hii, Aprili 19, na kwa wiki sita zijazo, Wahindi milioni 970 wanaitwa kupiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa wabunge. Chama au muungano utakaopata wingi wa viti katika Lok Sabha utaunda serikali ijayo. Na ni katika Kairana, kwenye mpaka wa magharibi wa jimbo la Uttar Pradesh, kaskazini mwa New Delhi, ambapo wapiga kura wa kwanza wanazungumza.

Wapiga kura wakisubiri kwenye foleni katika kituo cha kupigia kura huko Kairana, katika jimbo la Uttar Pradesh, kwa ajili ya uchaguzi wa wabunge nchini India, Aprili 19, 2024.
Wapiga kura wakisubiri kwenye foleni katika kituo cha kupigia kura huko Kairana, katika jimbo la Uttar Pradesh, kwa ajili ya uchaguzi wa wabunge nchini India, Aprili 19, 2024. REUTERS - Anushree Fadnavis
Matangazo ya kibiashara

Na mwandishi wetu maalum katika Kairana, Clea Broadhurst

Wapiga kura katika Kairana (jimbo la Uttar Pradesh), ambapo Chama cha Bharatiya Janata cha Waziri Mkuu Narendra Modi (BJP) kinatawala kwa sasa, ndio wanakuwa wa kwanza kupiga kura huku awamu ya kwanza ya uchaguzi wa wabunge ikianza nchini India. Kutakuwa na awamu saba kwa jumla, hadi Juni 1 siku hiyo ikiwemo.

Wakitokea shule iliyogeuzwa kuwa kituo cha kupigia kura, kwa siku ya leo Ijumaa Aprili 19, siku ambayo ni likizo kwa ajili ya ufunguzi wa uchaguzi, watu waliojitokeza kupiga kura wanaonyesha moja ya vidole vitano kilichowekwa rangi ya bluu, uthibitisho kuwa tayari wameshapiga kura. "Ni jukumu letu kupiga kura! Ni kwa ajili ya Waziri Mkuu wetu, tunapaswa kupiga kura ikiwa tunataka serikali tunayoitaka,” anaeleza Asgar.

Naye Khushnuma, mwanamke ambaye anaishi zaidi ya kilomita 100 kutoka Kairana, anasema ilikuwa muhimu kuchukua njia hii kutekeleza haki yake: “Ni wajibu wangu kupiga kura. Ndio maana nimekuja mapema leo asubuhi! Matumaini yangu ni kwamba tutakuwa na amani na kuishi kwa maelewano. "

Ikiwa Uttar Pradesh inatawaliwa na BJP, baadhi ya wapiga kura, kama Mohamad, wanaamini kuwa ni wakati wa mabadiliko, kwa sababu machoni pake, serikali inawagawanya tu Wahindu na Waislamu: "Ni muhimu kupiga kura, kwa sababu lazima tuhifadhi Katiba yetu. Leo, kuna matatizo mengi katika nchi yetu: mfumuko wa bei, ukosefu wa ajira, elimu, wakulima ... Kuna matatizo mengi sana, ndiyo sababu tunapaswa kupiga kura. "

Miungano miwili mikuu uso kwa uso

Uwezo mwingi umekusanywa kwa ajili ya uhaguzi huu; Helikopta 41, treni maalum 84 na karibu magari milioni moja vimetumwa kusafirisha maafisa wa uchaguzi na usalama. Kura imepangwa kwa muda wa siku 44 kwa sababu za vifaa na usalama. Mamilioni ya mashine za kielektroniki za kupigia kura zitatumika na zitawawezesha wapigakura kuchagua kati ya wagombea kadhaa… au kutochagua yeyote.

Kwa vile India ni demokrasia ya vyama vingi, uchaguzi utashuhudia vyama vingi vya kitaifa na kikanda vikishindana kwa kura. Lakini miungano miwili mikuu inashindana moja kwa moja kuongoza taifa: National Democratic Alliance (NDA), inayoongozwa na BJP ya Modi, na muungano wa vyama 26, uitwao Indian National Developmental Inclusive Alliance (INDIA), unaoongozwa na chama kikuu cha upinzani, India National Congress (INC).

Kwa jumla, majimbo 21 nchini India yanapiga kura mnamo Aprili 19 kwa viti 102 kati ya viti 543. Huko Uttar Pradesh, wanapigia kura viti 8 kati ya 80 vilivyopewa jimbo kwa jumla. Kwa viti hivi 8, kuna wagombea 80, wakiwemo wanawake saba. Upigaji kura unafanyika katika vituo 7,693 vya kupigia kura. Matokeo yote yatatolewa Juni 4.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.