Pata taarifa kuu

Burundi: Mwanahabari Sandra Muhoza ashtakiwa kwa kuhatarisha usalama wa nchi

Mwanahabari wa nchini Burundi ameshtakiwa kwa kosa la kuhatarisha usalama wa nchi, kosa ambalo anaweza kufungwa jela maisha, mawakili wake na familia wamethibitisha.

Alifunguliwa mashtaka siku ya Alhamisi na kuhamishiwa katika gereza maarufu la Mpimba mjini Bujumbura
Alifunguliwa mashtaka siku ya Alhamisi na kuhamishiwa katika gereza maarufu la Mpimba mjini Bujumbura AFP/Carl de Souza
Matangazo ya kibiashara

Idara ya kitaifa ya ujasusi ilimkamata Sandra Muhoza, 42, mwandishi wa habari wa mtandao wa La Nova Burundi, mwishoni mwa wiki iliyopita katika mji mkuu wa kiuchumi wa nchi hiyo Bujumbura.

Alifunguliwa mashtaka siku ya Alhamisi na kuhamishiwa katika gereza maarufu la Mpimba mjini Bujumbura.

Rais wa  Burundi, Évariste Ndayishimiye, amekuwa akisisitiza kuwa nchi yake inaheshimu haki za binadamu.
Rais wa Burundi, Évariste Ndayishimiye, amekuwa akisisitiza kuwa nchi yake inaheshimu haki za binadamu. AP - Peter Dejong

Vyombo vya usalama vilimkamata Muhoza baada ya maoni anayodaiwa kutoa katika kikundi cha WhatsApp cha waandishi wa habari wakijadili madai ya kusambaza silaha kwa Imbonerakure, wanachama wa kundi la vijana wa chama tawala CNDD-FDD, kulingana na wakili wake na watu wa familia yake.

Familia yake na mawakili wake wanadai kuwa Muhoza alifungwa macho na kufungwa pingu wakati akihojiwa pamoja na kupigwa na kunyimwa chakula madai ambayo hadi tukichapisha taarifa hii, mamlaka haikuwa imetoa taarifa yake kuyahusu.

Soma piaBurundi: Mwanahabari Sandra Muhoza anazuiliwa na idara ya ujasusi

Si mara ya kwanza kwa waandishi wa habari kulengwa nchini Burundi, taifa ambalo lina rekodi mbovu kuhusiana na masuala  ya uhuru wa vyombo vya habari na haki za binadamu.

Muungano wa waandishi wa habari nchini Burundi hapo jana Alhamisi ulisema kwamba unatumai Muhoza ataachiliwa huru na kuwataka waandishi wengine kuonyesha mshikamano naye wakati huu mgumu.

Shirika la Kimataifa linalotetea wanahabari la Reporters Without Borders.
Shirika la Kimataifa linalotetea wanahabari la Reporters Without Borders. AFP/Bertrand Guay

Haya yanajiri wakati huu muungano wa wanahabari wasio na mipaka Reporters Without Borders, RSF, ukielezea wasiwasi wake kuhusu kukamatwa na kuwekwa kizuizini kwa mwanahabari huyo.

Mwaka jana, RSF iliorodhesha Burundi katika nafasi ya 114 kati ya nchi 180 katika orodha ya nchi zilizo na rekodi mbaya kuhusu uhuru wa vyombo vya habari.

Hillary Ingati, RFI-Kiswahili/AFP.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.