Pata taarifa kuu
AFCON 2023

Patson Daka ainyima Tanzania ushindi wa kwanza michuano ya AFCON

San Pedro, Cote d'Ivoire – Bao la mshambuliaji wa Leicester City, Patson Daka dakika ya 88, alilounganisha kwa kichwa kutoka kwa kona ya Clatous Chama lilitosha kuwanyima Taifa Stars ushindi wao wa kwanza kwenye historia yao ya kushiriki michuano ya AFCON. Bao hilo aidha liliongeza matumaini ya Chipolopolo kutinga hatua ya 16 bora.

Mshambuliaji wa Zambia Patson Daka dhidi ya Tanzania uwanjani Laurent Pokou, San Pedro 21/01/2024
Mshambuliaji wa Zambia Patson Daka dhidi ya Tanzania uwanjani Laurent Pokou, San Pedro 21/01/2024 © CAF
Matangazo ya kibiashara

Simon Msuva aliiweka Tanzania kifua mbele dakika ya 11 baada ya kupokea pasi nyerezi kutoka kwa nahodha Ally Mbwana Samatta.

Zambia ilipata pigo baada ya beki Rodrick Kabwe kupokea kadi ya pili ya njano dakika ya 44 kwa kumchezea rafu Mbwana Samatta.

Hii ni sare ya tatu kwa Tanzania katika historia yao kwenye michuano hiyo baada ya sare ya kwanza dhidi ya Ivory Coast katika michuano ya mwaka 1980. Katika michuano ya mwaka 2019, Tanzania ilipoteza mechi zote tatu.

Mshambuliaji wa Tanzania Simon Msuva (aliyeruka) na Feisal Salum wakisherehekea baada ya kufunga bao dhidi ya Zambia
Mshambuliaji wa Tanzania Simon Msuva (aliyeruka) na Feisal Salum wakisherehekea baada ya kufunga bao dhidi ya Zambia © CAF

“Tulijua itakuwa mechi ngumu baada yao kupata kadi nyekundu. Ukosefu wa umakini dakika za mwisho imetuumiza,” alisema kocha Hemed Suleiman.

“Inabidi tuchukue matokeo, hatuwezi kubadilisha chochote. Bado tuna mchezo mmoja wa kupambana tupate ushindi ili tufuzu raundi inayofuata,” nahodha Mbwana Samatta.

Patson Daka ambaye alitajwa mchezaji bora wa mechi aliridhika na matokeo.

“Haikuwa mechi rahisi. Tanzania si wapinzani rahisi. Sare si mbaya sana lakini tungetaka zaidi kama tungekuwa wachezaji sawa uwanjani. Ila tugange yajayo.”

Daka kwenye mahojiano na wanahabari baada ya mechi dhidi ya Tanzania
Daka kwenye mahojiano na wanahabari baada ya mechi dhidi ya Tanzania © Jason Sagini

Kwa upande mwingine, kocha wa Zambia Avrant Grant alinyoshea kidole cha lawama maamuzi ya mechi hiyo.

“Kadi nyekundu aliyotoa refa, haikustahili sababu kandi ya njano ya kwanza haikufaa. Nafikiri CAF inafaa kuzingatia mambo kama haya.”

“Lakini hata na wachezaji kumi, mliona tulionesha viwango vya juu sana. Tungeshinda mechi ila Tanzania ni wagumu sana kucheza nao.”

Morocco na DRC walitoka sare ya 1-1 katika mchezo wa awali wa kundi hilo.

Huku Adel Amrouche akiwa hayupo akihudumia adhabu yake kutoka kwa Shirikisho la Soka Afrika (Caf) kutokana na matamshi aliyoyatoa kuhusu Morocco, kocha mkuu wa muda Hemed Suleiman Ali anaweza kuiongoza Tanzania hadi hatua ya mtoano kwa mara ya kwanza katika historia yao iwapo wataishinda DR Congo siku ya Jumatano nayo Zambia isiiduwaze Morocco katika mechi za mwisho za Kundi F, ingawa kushindwa kutawahakikishia kuondolewa kwao na sare haitawawezesha kuendeleza kampeni yao.

Zambia, ambao walitoka sare ya 1-1 na Leopards katika mechi yao ya kwanza, pia wanajua ushindi dhidi ya Morocco, utawarudisha katika hatua ya 16 kwa mara ya kwanza tangu kutwaa ubingwa wa Afcon 2012.

Pointi moja inaweza kuhitimisha maendeleo yao bila hitaji la kuwa moja ya timu nne bora zilizo katika nafasi ya tatu ikiwa mchezo mwingine utaisha kwa sare na kuzidisha idadi ya mabao yaliyofungwa na DR Congo.

 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.