Pata taarifa kuu

Tabianchi: Wataalamu wa UN washushia lawama kampuni kubwa ya mafuta ya Saudia Aramco

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wameishtumu, katika barua zilizotangazwa hadharani Jumamosi Agosti 26, kampuni kubwa ya mafuta ya Saudi Arabia Aramco kuhusu madhara ya shughuli yake juu ya ongezeko la joto duniani.

Mitambo ya  mafuta ya kampuni ya Aramco huko Jeddah, Saudi Arabia, mnamo 2021.
Mitambo ya mafuta ya kampuni ya Aramco huko Jeddah, Saudi Arabia, mnamo 2021. AP - Amr Nabil
Matangazo ya kibiashara

Barua hizi, zilizochapishwa kwenye mtandao miezi miwili baada ya kutumwa, zinadai kuwa wataalamu wa Umoja wa Mataifa wamepokea taarifa "kuhusu shughuli za kibiashara za kampuni ya Saudi Aramco (...) ambazo zina matokeo mabaya kwa ulinzi wa haki za binadamu katika muktadha wa mabadiliko ya tabianchi”. Hasa, wanashutumu kwa "kudumisha uzalishaji wa mafuta yasiyosafishwa, kuchunguza hifadhi mpya za mafuta na gesi, kupanua shughuli zake za gesi ya mafuta na habari zisizo sahihi".

'Saudi Aramco, msambazaji mkubwa wa gesi chafu'

Wataalam wa Umoja wa Mataifa wanabaini kwamba shughuli za biashara za Saudi Aramco zinaonekana "kinyume na malengo, wajibu na ahadi za mkataba wa Paris", unaolenga kupunguza ongezeko la wastani wa joto duniani hadi 1.5Β°C. Barua hizo kwa Aramco na wafadhili wake zilitumwa na wataalamu kutoka kikundi Kazi cha Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za kibinadamu na mashirika ya kimataifa, pamoja na waandishi Maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Kibinadamu na mabadiliko ya tabianchi.

Kulingana na barua hizi, nishati ya mafuta inawajibika kwa zaidi ya 75% ya uzalishaji wa gesi chafu duniani. Zinataja ripoti zinazokadiria kuwa zaidi ya nusu ya uzalishaji huu unaweza kuhusishwa na makampuni 25 katika sekta ya mafuta, "Saudi Aramco ikiwa msambazaji mkubwa zaidi wa gesi chafuzi".

Hakuna jibu

"Kwa hiyo, kutokana na uzalishaji wake wa kihistoria, Saudi Aramco ingekuwa tayari imechangia kwa kiasi kikubwa athari mbaya za haki za binadamu zinazohusiana na mabadiliko ya tabinchi." Wataalamu wa Umoja wa Mataifa ni watu huru, wasio na malipo ambao hawazungumzi kwa niaba ya Umoja wa Mataifa, lakini wanawajibika kuripoti matokeo yao kwa umoja huo. Barua hiyo imeitaka kampuni ya Aramco kutoa maoni yake kuhusu hoja kumi ndani ya siku 60, baada ya hapo barua na majibu yoyote yatakayopokelewa yatawekwa wazi.

Hakuna jibu kutoka kwa Aramco lililoonekana kwenye tovuti ya Umoja wa Mataifa ya taratibu maalum za haki za binadamu Jumapili asubuhi. Faida ya Aramco ndiyo chanzo kikuu cha ufadhili wa mpango mkubwa wa Mwanamfalme Mohammed bin Salman wa mageuzi ya kiuchumi na kijamii, yenye lengo la kuwezesha ufalme huo kuleta mseto wa uchumi wake, ambao kwa kiasi kikubwa unategemea nishati ya mafuta.

(Pamoja na AFP)

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.